September 28, 2011

Swala La Talaka Na Kuoa Tena


Swala La Talaka Na Kuoa Tena
Jambo la talaka na kuoa tena baada ya talaka hujadiliwa sana miongoni mwa Wakristo wa kweli. Yapo maswali mawili ambayo ndiyo msingi wa mjadala huo. (1) Ni wakati gani – kama upo – ambapo talaka inaruhusiwa machoni pa Mungu? Na (2) Ni wakati gani – kama upo – ambapo kuoa tena kunaruhusiwa machoni pa Mungu? Madhehebu mengi na makanisa binafsi yana msimamo rasmi kimafundisho kuhusu kinachoruhusiwa na kisichoruhusiwa, kutokana na tafsiri yao ya Maandiko. Tunapaswa kuwaheshimu wote kw akuwa na misimamo na kuishi kulingana nayo – ikiwa misimamo hiyo inasukumwa na kumpenda Mungu kwao. Hakika ingekuwa vizuri kama sisi wote tungekuwa na misimamo ambayo inaungwa mkono na Maandiko mia kwa mia. Mchungaji anayefanya wengine kuwa wanafunzi hataki kufundisha kitu kinachopungua kwenye kusudi la Mungu. Wala hataki kuweka mizigo juu ya watu, ambayo Mungu hakukusudia wao waibebe. Basi, hayo yakiwa hivyo, hebu nijitahidi kufasiri Maandiko yanayohusiana na mada hii tata, na kukuacha wewe uamue kama unakubaliana na tafsiri hiyo au hapana.
Nianze kwa kusema kwamba mimi – kama wewe – nahuzunishwa sana na ukweli kwamba talaka imezidi sana duniani siku hizi. Kibaya zaidi ni kwamba kuna Wakristo wengi wanaoachana na wenzao, hata walio katika huduma. Hili ni janga kubwa sana. Tunahitaji kufanya kila kinachowezekana ili kuzuia hayo kuongezeka, na ufumbuzi mzuri zaidi wa tatizo la talaka ni kuhubiri Injili na kuwaita watu kutubu. Wakati watu wawili wenye ndoa wanapokuwa wamezaliwa tena kweli kweli na wote wanamfuata Kristo, hawataachana. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi atafanya kila anachoweza kuimarisha ndoa yake, akijua kwamba mfano wa maisha yake ndiyo mwalimu mkuu.
Niseme pia kwamba mimi nina ndoa yenye furaha sana ya miaka zaidi ya ishirini na tano, na sijawahi kuoa kabla ya ndoa hii. Siwezi kufikiri kwamba tutakuja kuachana. Kwa hiyo, sina kusudi lolote la kurahisisha maandiko magumu yanayohusu kuachana kwa faida yangu mwenyewe. Ila, ninawahurumia sana watu walioachana, nikijua kwamba hata mimi nilipokuwa kijana ningeweza kufanya uamuzi mbaya kirahisi tu, na kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye baadaye ningejaribiwa sana kumwacha, au mtu ambaye asingeweza kuchukuliana nami kama huyu niliye na ndoa naye. Yaani, ningeishia kwenye talaka, lakini haijawa hivyo kwa sababu ya neema ya Mungu. Nadhani watu wengi wenye ndoa wanaelewa ninachosema. Basi, tunahitaji kujizuia tusitupe mawe kwa watu walioachana. Kwani sisi ni nani, wenye ndoa zisizo na matatizo sana, kuwahukumu walioachana, bila ya kujua wamepitia nini? Mungu anaweza kuwahesabu kuwa wenye haki kuliko sisi, maana anajua kwamba sisi, kama tungekuwa katika hali kama hizo, pengine tungevunja ndoa mapema zaidi.
Hakuna anayeoa akitazamia kuvunja ndoa, na sidhani kama kuna wanaochukia kuachana kama waliokwisha achana. Kwa hiyo, tujaribu kuwasaidia watu wenye ndoa kuendelea kuwa katika ndoa, na tuwasaidie walioachana kupata neema yoyote ile ambayo Mungu anaitoa kwa watu kama wao. Ninaandika ninayoandika kwa misingi hiyo.
Nitajitahidi sana kuruhusu maandiko yafafanue mengine. Nimeona kwamba mistari inayohusu mada hii mara nyingi hutafsiriwa kwa njia kwamba inapingana na Maandiko mengine, ambayo ni ishara kwamba haijaeleweka vizuri kwa sehemu.
Msingi
Hebu tuanze kwa kweli ya msingi ambayo sote tutakubaliana nayo. Ni hivi: Maandiko yanasema wazi kwamba Mungu hapendi kuachana kwa ujumla. Katika kipindi ambapo wanaume fulani wa KiIsraeli walikuwa wanatalakiana na wake zao, alitamka hivi kupitia nabii wake aitwaye Malaki:
Maana mimi nakuchukia kuachana … naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia … Basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana (Malaki 2:16).
Hilo si jambo la kushangaza kwa mtu yeyote ajuaye tabia ya Mungu ya upendo na haki, au mtu anayejua jinsi kuachana kunavyoharibu waume, wake na watoto. Mtu anayekubaliana na talaka kwa ujumla tungehoji tabia yake. Mungu ni upendo (ona 1Yohana 4:8), na kwa sababu hiyo anachukia talaka.
Kuna wakati fulani ambapo baadhi ya Mafarisayo walimwuliza Yesu swali kuhusu uhalali wa talaka “kwa sababu yoyote” (TLR). Jibu lake linaonyesha jinsi asivyokubali talaka. Tena, talaka halikuwa kusudi Lake kwa yeyote yule.
Basi Mafarisayo wakamwendea wakamjaribu wakimwambia, ‘Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?’ Akajibu akawaambia, ‘Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe’ (Mathayo 19:3-6).
Tunajua kihistoria kwamba yalikuwepo makundi mawili yaliyokuwa na mitazamo tofauti katika vongozi wa kidini wa Kiyahudi wakati wa Yesu. Tutatazama mitazamo ya makundi hayo mawili kwa upana zaidi baadaye, lakini kwa sasa inatosha tu kusema kwamba kundi moja lilikuwa na msimamo mkali na lingine msimamo mwepesi. Wenye msimamo mkali waliamini kwamba mwanamume aliruhusiwa kumwacha mkewe kwa sababu nzito sana kiadili. Wale wenye msimamo mwepesi waliamini kwamba mwanamume aliruhusiwa kumwacha mkewe kwa sababu yoyote ile, hata kama amempata mwanamke mrembo zaidi. Mitazamo hiyo miwili tofauti ndiyo ilisababisha swali la Mafarisayo kwa Yesu.
Yesu akarejea kwenye mistari ya Maandiko kutoka kurasa za kwanza kabisa za kitabu cha Mwanzo, yenye kuonyesha jinsi ambavyo mpango wa kwanza wa Mungu ulikuwa kuwaunganisha wanaume na wanawake pamoja daima, si kwa muda tu. Musa alisema kwamba Mungu aliumba jinsia hizo mbili akilenga ndoa, na kwamba ndoa ni uhusiano wa maana sana kiasi cha kwamba ndiyo wa msingi – au, ndiyo wa kwanza kabisa. Ukiisha undwa, ni wa hali ya juu kuliko mahusiano ya mtu na wazazi wake. Wanaume wanaachana na wazazi wao ili kuambatana na wake zao.
Tena, muungano wa kimwil katika tendo la ndoa baina ya mwanamume na mkewe huonyesha mpango wa Mungu kwao kwamba wawe mwili mmoja. Ni dhahiri kwamba uhusiano wa aina hiyo – ambao unasababisha kuzaa – haukukusudiwa na Mungu uwe wa muda, bali wa kudumu. Jinsi Yesu alivyojibu swali la Mafarisayo lilionyesha kuvunjwa moyo Kwake kwamba wamediriki kuuliza hata swali la aina hiyo. Hakika Mungu hakukusudia kwamba wanaume waachane na wake zao “kwa sababu yoyote.”
Mungu hakukusudia kwamba yeyote atende dhambi kwa namna yoyote ile, lakini wote tumefanya dhambi. Kwa rehema zake, Mungua liweka mpango wakutuokoa kutokana na utumwa wetu wa dhambi. Tena, ana mambo ya kutuambia baada ya kufanya yale ambayo hakutaka tuyafanye. Vivyo hivyo, Mungu hakukusudia mtu yeyote aachane na mwenzake, lakini talaka ikawa haiepukiki kwa watu wasiojitoa kwa Mungu. Mungu hakushangazwa na talaka ya kwanza, wala zile zilizofuata kwa mamilioni. Basi, hasemi tu kwamba anachukia kuachana, lakini pia ana mambo ya kuwaambia watu baada ya kuachana.
Hapo Mwanzo
Baada ya kuweka msingi, tunaweza sasa kuendelea kuchunguza zaidi mambo ambayo Mungu amesema kuhusu talaka na kuoa tena. Kwa kuwa maneno mengi yenye kuleta utata kuhusu talaka na kuoa tena ni yale ambayo Yesu aliwaambia Waisraeli, itatusiadia kwanza kuona Mungu alichosema miaka mia nyingi kabla, juu ya jambo hilo hilo kwa Waisraeli wa zamani. Tukikuta kwamba alichosema Mungu kwa njia ya Musa na alichosema Mungu kwa njia ya Yesu vinapingana, basi tujue kwamba sheria ya Mungu ilibadilika au kwamba sisi tumetafsiri isivyo kitu fulani kilichosemwa na Musa au na Yesu. Basi, tuanze kwa kutazama yale ambayo Mungu alifunua hapo mwanzo kuhusu talaka na kuoa tena baada ya talaka.
Tayari nimekwisha taja Maandiko ya Mwanzo 2 ambayo kulingana na Yesu, yana umuhimu kwa mada ya talaka. Hebu sasa tuyaone moja kwa moja kutoka Mwanzo kwenyewe.
Na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, ‘Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kw ahiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja (mwanzo 2:22-24).
Basi huo ndiyo mwanzo wa ndoa. Mungu alimfanya mwanamke wa kwanza kutoka kwa mwanamume wa kwanza, na kwa ajili ya mwanamume wa kwanza, kisha Yeye Mwenyewe binafsi akamleta kwa Adamu. Yesu anaeleza hilo hivi, “Mungu … aliwaunganisha [pamoja]” (Mathayo 19:6, maneno mepesi kutilia mkazo). Hii ndoa ya kwanza iliyopangwa na Mungu ikatoa mfano kwa ajili ya ndoa zingine zote zilizofuata. Mungu huumba wanawake wa kutosha wanaume, Naye huwaumba ili kila mmoja avutiwe na mwenzake. Tunaweza kusema kwamba Mungu bado anapanga ndoa za watu kwa hali ya juu sana (japo siku hizi kuna wanaoweza kuwa wenzi wengi zaidi kwa kila mtu kuliko ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa). Basi, kama Yesu alivyosema, mwanadamu yeyote asitenganishe wale ambao Mungu amewaunganisha. Halikuwa kusudi la Mungu kwamba wale wana ndoa wa kwanza waishi maisha binafsi kila mmoja, bali kwamba wapate baraka katika kuishi pamoja kwa hali ya kutegemeana. Kuhalifu mapenzi ya Mungu yaliyo dhahiri ni dhambi. Basi, kutoka katika sura ya pili ya Biblia, ukweli ni kwamba talaka haikuwa kusudi la Mungu kwa ndoa yoyote ile.
Sheria Za Mungu Kuandikwa Mioyoni
Pia niseme kwamba hata wale ambao hawajawahi kusoma sura ya pili ya Mwanzo wanajua ndani yao kwamba talaka ni kosa, kwa sababu agano la ndoa za maisha ni kawaida katika tamaduni nyingi tu za kipagani, ambapo hakuna maarifa yoyote ya Biblia. Kama alivyoandika Paulo katika barua yake kwa Warumi:
Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao wakionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao yenyewe kwa yenyewe, yakiwashtaki au kuwatetea (Warumi 2:14-15).
Taratibu za Mungu za maadili zimeandikwa katika moyo wa kila mwanadamu. Ukweli ni kwamba kanuni hiyo ya maadili inayozungumza kupitia dhamiri ndiyo sheria pekee ambayo Mungu aliwahi kumpa yeyote, isipokuwa Waisraeli, tangu Adamu mpaka wakati wa Yesu. Yeyote anayefikiri talaka atagundua kwamba kuna dhamiri ya kushughulika nayo. Na njia ya pekee ya kuishinda dhamiri yake ni kutafuta haki nzuri kwa ajili ya talaka. Akiendelea na talaka bila ya haki nzuri, dhamiri yake itamshtaki, hata kama atajaribu kuigandamiza.
Kwa kadiri tunavyofahamu, tangu Adamu mpaka wakati wa kutolewa Torati ya Musa kwa Waisraeli mwaka wa 1440 KK, sheria ya dhamiri ndiyo ufunuo pekee ambao Mungu alitoa kwa yeyote kwa vizazi 27 hivi – hata kwa Waisraeli – kuhusiana na talaka na kuoa tena. Na Mungu alihesabu kwamba hiyo inatosha. (Kumbuka tu kwamba Musa hakuandika habari za uumbaji katika Mwanzo 2 mpaka wakati wa Kutoka Misri.) Basi, ni halali kabisa kufikiri kwamba katika kipindi cha vizazi hivyo 27 kabla ya Torati ya Musa – ambapo ni pamoja na kipindi cha gharika ya Nuhu – kiasi fulani cha ndoa katika zile milioni nyingi za miaka mia nyingi zilimalizika kwa kuachana. Pia inaonekana ni sawa kusema kwamba, Mungu asiyebadilika, alikuwa tayari kuwasamehe wale waliopatikana na hatia ya talaka kama walitubu na kuacha dhambi yao. Tuna hakika kwamba watu walikuwa wanaokoka au kutangazwa kuwa wenye haki na Mungu kabla ya Torati ya Musa kutolewa, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu kwa imani yake (ona Warumi 4:1-12). Kama watu waliweza kutangazwa kuwa wenye haki kwa njia ya imani yao – tokea Adamu hadi kwa Musa – maana yake ni kwamba wangeweza kusamehewa chochote, pamoja na dhambi ya talaka. Basi, tunapoanza kuchunguza swala la talaka na kuoa tena baada ya talaka, kuna swali hapa: Je, watu waliopatikana na dhambi katika talaka zao kabla ya Torati ya Musa, waliosamehewa na Mungu, waliweza kuhukumiwa na dhamiri zao na kupata hatia kama wangeoa tena? (Maana haikuwepo sheria iliyoandikwa.) Ni swali la kufikiri.
Vipi kuhusu wahanga wa talaka ambao hawakuwa na dhambi – yaani, walioachwa kwa kosa lisilokuwa lao, bali kwa sababu ya wenzi wenye ubinafsi? Je, dhamiri zao zingewazuia kuoa tena? Nadhani si hivyo. Kama mwanamume alimwacha mke wake kwa sababu ya mwanamke mwingine, nini kingemwongoza huyo mwanamke aliyeachwa kufikia uamuzi kwamba hana haki ya kuolewa tena? Maana, aliachwa, lakini si kosa lake.
Torati Ya Musa
Hatusomi habari za talaka na kuoa tena baada ya talaka mpaka tunapofikia kitabu cha tatu cha Biblia. Katika Torati ya Musa kulikuwa na agizo la kuwakataza makuhani kuona wanawake walioachwa.
Wasimwoe mwanamke aliye kahab, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake (Walawi 21:7).
Hakuna popote katika Torati ya Musa penye katazo la namna hiyo kwa wanaume wengine wa Israeli kwa ujumla. Tena, andiko hilo linabeba yafuatayo: (1) Walikuwepo wanawake waliokuwa wameachika katika Israeli, na (2) Kusingekuwepo kosa lolote kwa wanaume Waisraeli ambao si makuhani kuoa wanawake waliokuwa wameachika. Sheria inayotajwa katika mstari huo inawahusu makuhani tu na wanawake walioachika, wanaotaka kuolewa na makuhani. Hapakuwa na ubaya wowote katika Torati ya Musa kwa mwanamke yeyote aliyeachika kuolewa tena, mradi tu hakuolewa na kuhani. Na hakukuwa na kosa lolote kwa mwanamume, kuoa mwanamke aliyeachika, mradi si kuhani.
Kuhani mkuu (pengine kwa sababu ni mfano wa Kristo) alitakiwa kuishi kwa viwango vya juu zaidi kuliko hata makuhani wa kawaida. Yeye hakuruhusiwa hata kuoa mjane. Mistari kadhaa baadaye tunasoma hivi katika Walawi:
Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe (Walawi 21:14).
Je, andiko hili linathibitisha kwamba ilikuwa dhambi kwa wajane wote wa Israeli kuolewa tena, au kwamba ilikuwa dhambi kwa wanaume wote wa Israeli kuoa wajane? Hapana! Mstari huu unasema – tena kwa nguvu sana – kwamba isingekuwa dhambi kwa mjane yeyote kuolewa na mwanamume yeyote, mradi si kuhani mkuu. Tena unasema mwanamume mwingine yeyote alikuwa huru kuoa mjane, mradi si kuhani mkuu. Maandiko mengine yanathibitisha uhalali wa wajane kuolewa tena (ona Warumi 7:2-3; 1Timo. 5:14).
Mstari huo vile vile unaonyesha kwamba kusingekuwa na kosa lolote kwa mwanamume yeyote Mwisraeli kuoa mwanamke aliyeachika, au hata mwanamke ambaye hakuwa bikira – “aliyenajisika katika ukahaba” – mradi si kuhani au kuhani mkuu. Hoja hiyo inaungwa mkono na Walawi 21:7 pia. Tena, unasema kwamba katika Torati ya Musa, hapakuwa na kosa lolote kwa mwanamke aliyeachika kuolewa tena, au mwanamke “aliyenajisika katika ukahaba” kuolewa, mradi tu asiolewe na kuhani. Kwa neema sana, Mungu aliwapa wazinzi na walioachika nafasi nyingine, japo alikuwa kinyume kabisa na uzinzi na talaka.
Katazo La Pili Lililo Dhahiri Kinyume Cha Kuoa Tena
Je, Mungu alitoa “nafasi nyingine” ngapi kwa wanawake walioachika? Je, tuamue kwamba Mungu aliwapa wanawake walioachika nafasi moja zaidi katika Torati ya Musa, akiwaruhusu kuolewa tena mara moja tu? Huo ni uamuzi usio sahihi. Tunasoma hivi baadaye katika Torati ya Musa,
Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake na kumtoa katika nyumba yake. Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine. Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha na kumpa mkononi mwake na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa aliyemtwaa kuwa mkewe; yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za BWANA; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo BWANA Mungu wako, iwe urithi (Kumbu. 24:1-4).
Ona kwamba katika mistari hii, kitu kinachokatazwa peke yake ni yule mwanamke aliyeachika mara mbili (au aliyeachika mara moja na kuwa mjane mara moja) kuolewa tena na mumewe wa kwanza. Hakuna kinachosemwa kwamba ana hatia kwa sababu ameolewa mara ya pili. Na baada ya kuachika mara ya pili (au kuwa mjane kwa mume wake w apili), alichokatazwa tu ni kumrudia mumewe wa kwanza. Ni kwamba, angekuwa huru kuolewa na mwanamume mwingine yeyote (ambaye yuko tayari kujaribu bahati yake!). Ingekuwa ni dhambi kwake kuolewa na mtu mwingine yeyote, kusingekuwepo haja kwa Mungu kutoa maagizo hayo ambayo ni wazi kabisa. Kitu cha pekee ambacho Mungu angesema ni hiki: “Watu walioachika hawaruhusiwi kuoa au kuolewa tena.”
Tena – Kama Mungu alimruhusu mwanamke aina hii kuolewa mara ya pili, basi yule mwanamume aliyemwoa baada ya kuachika mara ya kwanza asingekuwa na hatia yoyote. Na kama aliruhusiwa kuolewa mara ya tatu, basi mwanamume yeyote ambaye angemwoa baada ya kuachika mara mbili asingekuwa na dhambi (isipokuwa kama alikuwa ndiye mumewe wa kwanza). Basi – Mungu anayechukia talaka anawapenda watu walioachika, na kwa rehema aliwapa nafasi nyingine.
Hitimisho
Hebu kwa muhtasari tuone yale ambayo tumejifunza mpaka hapa. Hata ingawa Mungu alitangaza kwamba anachukia t alaka, hakuonyesha kabla au wakati wa agano la kale kwamba kuoa na kuolewa tena ni dhambi, isipokuwa katika haya mawili yafuatayo: (1) mwanamke aliyeachika mara mbili – au aliyeachika mara moja na kufiwa na mume wa pili – kuolewa na mumewe wa kwanza, na (2) mwanamke aliyeachika kuolewa na kuhani. Tena, Mungu hakuonyesha kwamba kumwoa aliyeachika ni dhambi kwa yeyote, isipokuwa makuhani.
Hayo yanaonekana kupingana na yale Yesu aliyosema juu ya watu walioachika wanao-oa tena, na wale wenye kuoa walioachika. Yesu alisema watu kama hao wanazini (ona Mathayo 5:32). Basi, yaonekana tumemwelewa vibaya Yesu au Musa, au pengine Mungu alibadilisha sheria Yake. Mimi nadhani tunaweza kuwa tunatafsiri vibaya yale aliyofundisha Yesu, kwa sababu ni ajabu kwa Mungu kutangaza ghafula kitu kuwa dhambi kiadili, kilichokuwa kinakubalika kwa miaka elfu na mia tano katika Torati ambayo Yeye aliitoa kwa Israeli.
Kabla ya kukabiliana na hili kwa upana zaidi, hebu pia tuone kwamba ruhusa ya Mungu kwa watu kuoa tena katika agano la kale haikuwa na masharti yoyote yaliyotokanana sababu za talaka ya mtu, au kiwango cha hatia ambacho mtu alipata kwa sababu ya talaka husika. Mungu hakusema kwamba watu fulani walioachika hawaruhusiwi kuoa au kuolewa kwa sababu talaka yao haikuwa halali. Hakusema kwamba kuna watu fulani wanaoruhusiwa kuona kwa sababu ya uhalali wa talaka zao. Lakini mara nyingi wachungaji wa siku hizi wanajaribu kufanya maamuzi hivyo, kutokana na ushuhuda wa mtu mmoja. Kwa mfano: Mwanamke aliyeachika anajaribu kumshawishi mchungaji wake kwamba anastahili kuruhusiwa kuolewa kwa sababu yeye ni mwathirika wa talaka. Mume wake wa kwanza ndiye alimwacha – si yeye. Lakini, kama huyo mchungaji atapewa nafasi ya kusikiliza upande wa mume naye, anaweza kumhurumia kwa namna fulani. Pengine huyo mama alikuwa mkorofi na anastahili lawama kiasi fulani.
Mimi najua mume na mke ambao wote wawili walijitahidi kukorofishana ili mmoja atoe talaka, kusudi waepukane na hatia kwamba ndio walioanzisha talaka. Wote walitaka waweze kusema baada ya kuachana kwamba, ni yule mwingine ndiye aliyeanzisha, na kwa njia hiyo, kuhalalisha ndoa zao za pili. Twaweza kuwadanganya watu, lakini hatuwezi kumdanganya Mungu. Kwa mfano: Mungu anamwonaje mwanamke ambaye anamnyima mumewe huduma za kitandani kila wakati, kisha anamwacha kwa sababu amekosa uaminifu kwake? Je, hahusiki na hiyo talaka kwa sehemu?
Lile jambo la mwanamke aliyeachika mara mbili katika Kumbukumbu 24 halisemi chochote kwamba talaka zake zote mbili ni halali. Mume wake wa kwanza aliona “neno ovu” kwake. Kama hilo “neno ovu” ni uasherati, angestahili kufa kulingana na Torati ya Musa (Walawi 20:10). Basi, kama uasherati tu ndiyo sababu halali ya talaka, pengine mume wake wa kwanza hakuwa na sababu nzuri ya kumwacha. Kwa upande wa pili, pengine alikuwa amezini, naye, akiwa mtu mwenye haki kama Yusufu wa Mariamu, “aliazimu kumwacha kwa siri” (Mathayo 1:19). Hapo kuna mengi yanayowezekana.
Mume wa pili anasemekana “akimchukia”. Hapa tena, hatujui wa kulaumiwa ni nani, au hata kama wote wanastahili kulaumiwa. Lakini bado haiweki tofauti. Neema ya Mungu ilitolewa kwake kwamba aolewe na yeyote ambaye angekubali kujaribu bahati yake kwa mwanamke aliyeachika mara mbili, isipokuwa mume wake wa kwanza.
Pingamizi
Watu mara nyingi wamesema hivi: “Kama watu wataambiwa ni halali kwao kuoa tena baada ya kuachana kwa sababu yoyote, itawatia moyo wao kuachana kwa sababu zisizo halali.” Yawezekana ikawa kweli kiasi fulani kwa watu wa dini ambao hawajitahidi kumpendeza Mungu. Lakini, kujaribu kuwazuia watu ambao hawajajitoa kwa Mungu kabisa wasitende dhambi ni swala gumu. Ila, watu waliojitoa kwa Mungu kabisa hawatafuti njia za kutenda dhambi. Wanajaribu kumpendeza Mungu. Na watu aina hiyo kwa kawaida wana ndoa zenye nguvu. Tena, Mungu hakusumbuka sana kwamba watu katika agano la kale wataachana kwa sababu zisizo halali kwa sababu ya kuwapa sheria nyepesi ya kuoa au kuolewa tena, maana sheria aliyotoa kwa Israeli kuhusu jambo hilo ilikuwa nyepesi kabisa.
Je, tuepuke kuwaambia watu kwamba Mungu yuko tayari kuwasamehe dhambi yoyote, wasije wakatiwa moyo kutenda dhambi kwa sababu wanajua msamaha unapatikana? Kama ndivyo, itabidi tuache kuhubiri Injili. Kila kitu kinategemea hali ya moyo ya wanadamu. Wale wanaompenda Mungu wanataka kumtii. Ninajua vizuri sana kwamba msamaha wa dhambi unapatikana kwangu nikiomba, hata kama nitatenda dhambi gani. Lakini hiyo hainisukumi kufanya dhambi hata kidogo, kwa sababu nampenda Mungu na nimezaliwa mara ya pili. Nimebadilishwa kwa neema ya Mungu. Ninataka kumpendeza.
Mungu anajua hakuna haja ya kuongeza tokeo lingine baya kwenye matokeo mabaya mengi yasiyoepukika ya talaka, kwa matumaini ya kuwahamasisha watu wakae katika ndoa. Kuwaambia watu wenye ndoa zenye shida kwamba wasiachane kwa sababu hawataruhusiwa kuoa au kuolewa tena hakutoi hamasa kwa watu kuendelea katika ndoa. Hata kama atakuamini, uwezekano wa kuishi peke yake ukilinganisha na maisha ya mateso ya ndoa daima utasikika kama paradiso kwa mtu mwenye ndoa mbaya.
Asemavyo Paulo Kuhusu Kuoa Tena
Kabla ya kupambana na tatizo la kulinganisha maneno ya Yesu nay a Musa kuhusu kuoa tena, tunahitaji kutambua kwamba yupo mwandishi mwingine mmoja wa Biblia anayekubaliana na Musa, naye ni Paulo Mtume. Paulo aliandika waziwazi kabisa kwamba kuoa au kuolewa tena kwa walioachika si dhambi, na kukubaliana na kinachosemwa na Agano la Kale.
Kwa habari za wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu. Basi naona hili kuw ajema kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo. Je, umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke. Lakini kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia. Lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo (1Wakor. 7:25-28. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Bila shaka Paulo alikuwa anasema na watu walioachika katika fungu hili. Anawashauri walio na ndoa, wasio na ndoa na walioachika wabaki katika hali zao kwa sababu ya mateso ambayo Wakristo walikuwa wanapitia wakati huo. Ila, Paulo alisema wazi wazi kwamba watu walioachika na wanawali hawatatenda dhambi wakiingia katika ndoa.
Ona kwamba Paulo hafafanui uhalali wa kuoa au kuolewa tena kwa walioachika. Hakusema kwamba kuoa au kuolewa tena kunaruhusiwa kama walioachika hawana lawama yoyote katika talaka ya ndoa iliyopita. (Kwani, nani mwenye sifa za kutosha kuhukumu kitu kama hicho, zaidi ya Mungu?) Hakusema kwamba kuoa au kuolewa tena kunaruhusiwa tu kwa wale ambao waliachana kabla ya kuokoka. Hapana! Yeye alisema tu kwamba kuoa au kuolewa tena si dhambi, kwa walioachika.
Je, Paulo Alilegeza Masharti Kuhusu Talaka?
Je, ina maana Paulo alilegeza masharti kuhusu talaka kwa kuwa aliruhusu kanuni ya neema kwa habari ya kuoa na kuolewa tena? Hapana! Paulo alikuwa anapingana na talaka kwa ujumla. Katika mistari ya mwanzoni ya sura hiyo hiyo ya barua ya kwanza kwa Wakorintho, aliweka sheria kuhusu talaka ambayo inalingana na chuki ya Mungu kwa talaka.
Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi ila Bwana; mke asiachane na mumewe. Lakini ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe. Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye, asimwache. Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi, bali sasa ni watakatifu. Lakini, yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyu ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani. Kwa maana wajuaje wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo? Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungualivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote (1Wakor. 7:10-17).
Angalia kwamba Paulo anasema na waamini kwanza, ambao wana ndoa na waamini wenzao. Hawapaswi kuachana, na Paulo anasema hayo si maagizo yake, bali ya Bwana. Bila shaka hayo yanakubaliana kabisa na kila kitu tulichotazama katika Biblia mpaka hapa.
Yanayofuata yanasisimua. Paulo alikuwa mkweli wa kutosha kutambua kwamba hata waamini wanaweza kuachana, japo kwa nadra. Hayo yakitokea, Paulo anasema kwamba yule aliyemwacha mwenzake akae bila ndoa au wapatane. (Japo ushauri wa Paulo unawalenga zaidi wake, kanuni hiyo bila shaka inawahusu hata waume.)
Hapa tena – alichoandika Paulo kisitushangaze. Anatangulia kuweka sheria ya Mungu kwanza kuhusu talaka, lakini ana akili ya kutosha kutambua kwamba kutii sheria ya Mungu si kitu kinachofanyika kila wakati. Hivyo, dhambi ya kuachana inapotokea kati ya waamini wawili, anatoa maagizo zaidi. Yule aliyemwacha mwenzake abaki bila kuoa au apatane na mwenzake. Hicho ndicho kinachofaa endapo waamini wawili wataachana. Muda wote watakaobaki hawana ndoa, kuna tumaini la wao kupatana, na hilo ndiyo bora. Kama mmoja wao akioa tena, hapo ndiyo mwisho wa matumaini na uwezekano wa kupatana. (Tena, kama wametenda dhambi isiyosameheka kwa kuachana, isingekuwepo sababu ya Paulo kuwaaambia wabaki bila ndoa au wapatane.)
Unaonaje? Paulo alikuwa na akili za kutosha kujua kwamba agizo lake la pili kwa waamini walioachana halitafuatwa? Bila shaka! Labda ndiyo sababu hakutoa ushauri zaidi kwa waamini walioachana kwa sababu alitazamia kwamba waamini wa kweli wangefuata agizo lake la kwanza la kutoachana, na kwamba katika mazingira adimu sana, agizo lake la pili lingehitajika. Kwa hakika, wafuasi wa kweli wa Kristo wangefanya kila kinachowezekana ili kuhifadhi ndoa yao, kama walikuwa na matatizo ya ndoa. Na kwa hakika, mwamini ambaye, baada ya juhudi zote za kuhifadhi ndoa angejisikia kwamba hana jinsi isipokuwa kuachana, kutokana na aibu yake binafsi na shauku ya kumheshimu Kristo asingefikiri kuwa na ndoa nyingine, na bado angetumainia mapatano. Inaonekana kwamba tatizo halisi katika kanisa la kisasa kuhusu talaka ni kwamba kuna waamini bandia wengi sana – watu ambao hawajawahi kumwamini Bwana Yesu kweli, na kujitoa kwake.
Ni dhahiri basi kutokana na yale Paulo anayoandika katika 1Wakorinto 7 kwamba, Mungu ana matazamio makubwa sana kwa waamini – watu waliojazwa na Roho Mtakatifu – kuliko aliyo nay kwa wasioamini. Kama tulivyosoma, Paulo aliandika kwamba waamini wasiwaache hata wenzao wasioamini mradi wako tayari kuishi nao. Hapo tena, agizo hili halitushangazi kwa sababu linakubaliana kabisa na kila kitu tulichosoma katika Manadiko kuhusu jambo hilo hadi sasa. Mungu anapinga talaka. Lakini Paulo anaendelea kusema kwamba, kama yule asiyeamini anataka talaka, mwamini aruhusu hiyo. Paulo anajua kwamba asiyeamini hajajitolea kwa Mungu, na hivyo hamtazamii asiyeamini kutenda kama anayeamini. Nyongeza ndogo hapo: Asiyeamini anapokubali kuishi na aaminiye, ni ushuhuda mzuri kwamba, pengine asiyeamini ana mwelekeo wa kupokea Injili, au yule anayeamini amerudi nyuma au ni Mkristo bandia.
Sasa, nani atakayesema kwamba mwamini aliyeachwa na asiyeamini hayuko huru kuoa tena? Paulo hasemi hivyo kamwe, kama alivyosema kwa habari ya waamini wawili walioachana. Itabidi kushangaa ni kwa nini Mungu apinge mwamini aliyeachwa na asiyeamini kuoa au kuolewa tena. Hilo lingetimiza kusudi gani? Lakini, ruhusa hiyo inaonekana inapingana na maelezo ya Yesu kuhusu kuoa tena, kwamba, “Yeyote amwoaye mwanamke aliyeachwa, azini” (Mathayo 5:32, TLR). Hapo tena, kuna mashaka kwamba pengine tumefasiri vibaya yale ambayo Yesu anasema.
Tatizo Lenyewe
Ni wazi kwamba Yesu, Musa na Paulo wanakubaliana kwamba kuachana au talaka ni dhihirisho la dhambi kwa mhusika mmoja au wote wawili. Wote wanapinga talaka kwa ujumla. Lakini tatizo letu ni hili: Tunaowanishaje yale ambayo Musa na Paulo wanasema kuhusu kuoa tena, na yanayosemwa na Yesu kuhusu jambo hilo hilo? Ni sawa tukitazamia kwamba yatalingana kwa sababu wote walivuviwa na Mungu kusema waliyosema.
Hebu tutazame kwa uhakika kwamba Yesu alisema nini, na tuwaone aliowaambia hayo. Katika Injili ya Mathayo, tunamwona Yesu mara mbili akisema jambo la talaka na kuoa tena – mara ya kwanza katika Hotuba ya Mlimani, na mara nyingine alipohojiwa na Mafarisayo fulani. Tuanze na mazungumzo ya Yesu na Mafarisayo hao.
Basi Mafarisayo wakamwendea wakamjaribu wakimwambia, ‘Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?’ Akajibu akawaambia, ‘Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.’ Wakamwambia, ‘Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?’ Akawaambia, ‘Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uahserati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa, azini’ (Mathayo 19:3-9).
Katika mazungumzo yao na Yesu, Mafarisayo walirejea Maandiko katika Torati ya Musa, ambayo tulikwisha yatazama mapema – Kumbukumbu la Torati 24:1-4. Hapo imeandikwa hivi: “Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake” (Kumbu. 24:1, Maneno mepesi kutilia mkazo).
Katika siku za Yesu yalikuwepo makundi mawili kimtazamo, kuhusu hicho kinachoitwa “neno ovu.” Miaka kama ishirini kabla ya swali hilo kuulizwa, mwalimu mmoja aliyeitwa Hileli alifundisha kwamba neno ovu lilikuwa ni tofauti isiyorekebika. Wakati huu ambapo Yesu anafanya majadiliano na Mafarisayo, tafsiri ya “Hileli” ilikuwa imepanuliwa sana na kuwa nyepesi mno, ikiruhusu talaka kwa “sababu yoyote” kama swali la Mafarisayo lilivyotoka. Mtu aliweza kumwacha mkewe kama ameunguza chakula, au chumvi ikizidi kwenye chakula, au kama alijizungusha sana mbele za watu magoti yake yakaonekana, au kama aliruhusunywele zake kuonekana, au kama alizungumza na mwanamume mwingine, au kama alisema maneno mabaya kuhusu mama mkwe wake, au kama alikuwa tasa. Mwanamume aliruhusiwa hata kumwacha mkewe kama angemwona mwingine ambaye ni mrembo zaidi – hivyo kuona “neno ovu” kwa mkewe.
Mwalimu mwingine maarufu aliitwa Shammai. Yeye aliishi kabla ya Hileli, na alifundisha kwamba “neno ovu” lilikuwa kitu kibaya sana, kama vile uzinzi. Bila shaka utatambua kwamba miongoni mwa Mafarisayo wa siku za Yesu, tafsiri ya Hileli ndiyo ilipendwa zaidi kuliko ya Shammai. Mafarisayo waliishi na kufundisha kwamba talaka ilikuwa halali kwa sababu yoyote. Basi, talaka iliongezeka sana. Na Mafarisayo – kama kawaida yao kiFarisayo – walikazia sana umuhimu wa kumpa mke hati ya talaka unapomwacha, ili usi”halifu Torati ya Musa.”
Usisahau Kwamba Yesu Alikuwa Anazungumza Na Mafarisayo
Baada ya kujua hayo, tutaelewa vizuri zaidi kilichokuwa kinamkabili Yesu. Mbele yake walisimama kundi la waalimu wa dini wanafiki, wengi ambao – kama si wote basi – walikuwa na talaka moja au zaidi, na pengine ni kwa sababu walikuwa wamepata wanawake warembo zaidi. (Si bahati kwamba maneno ya Yesu kuhusu talaka katika Mahubiri ya Mlimani yanafuata maonyo Yake makali sana kuhusu tamaa, na kusema ni aina ya uzinzi.) Na bado walikuwa wanajihesabia haki, wakidai kwamba wameishika Torati ya Musa.
Swali lao tu linadhihirisha jinsi walivyoegemea upande mmoja. Waliamini kabisa kwamba mtu angeweza kumwacha mke wake kwa sababu yoyote. Yesu akadhihirisha ufahamu wao mbovu wa kusudi la Mungu kuhusu ndoa kwa kurejea maneno ya Musa juu ya ndoa katika Mwanzo sura ya 2. Mungu hakukusudia kuwepo na talaka zozote, achilia mbali talaka “kwa sababu yoyote,” lakini viongozi wa Israeli walikuwa wanawaacha wake zao kiholela tu!
Inaonekana Mafarisayo walijua tayari msimamo wa Yesu kuhusu talaka, maana alikwisha kuutamka hadharani. Basi wakawa na pingamizi tayari: “Mbona basi Musa aliagiza apewe hati ya talaka na kumwacha?” (Mathayo 19:7, TLR).
Hapo tena swali lao linaonyesha jinsi walivyogemea upande mmoja. Limeulizwa kana kwamba Mus aalikuwa anawaagiza wanaume wawaache wake zao baada ya kugundua “neno ovu,” mradi tu watoe hati ya talaka. Lakini, kama tujuavyo kutokana na Kumbukumbu 24:1-4, Musa hakusema hivyo hata kidogo. Yeye alikuwa anaweka sawa ndoa ya tatu ya mwanamke – akimzuia asiolewe tena na mume wake wa kwanza.
Kwa vile Musa alitaja talaka, bila shaka talaka ilikuwa inaruhusiwa kwa sababu fulani. Lakini ona kwamba neno alilotumia Yesu katika jibu lake – aliruhusu – ni tofauti na chaguo la Mafarisayo – aliamuru. Musa aliruhusu talaka, hakuamuru. Na sababu ya Musa kuruhusu talaka ni ugumu wa mioyo ya Waisraeli. Yaani – Mungu aliruhusu talaka kama tendo la huruma tu kwa hali ya dhambi ya watu. Alijua watu wasingekuwa waaminifu kwa wana ndoa wenzao. Alijua uchafu ungekuwepo. Alijua mioyo ya watu ingevunjika. Basi, akatoa ruhusa kwa talaka. Hakuwa amekusudia hivyo tangu mwanzo, lakini dhambi ililazimisha hivyo.
Kisha Yesu akaweka sheria ya Mungu wazi kwa Mafarisayo, akifafanua kile ambacho Musa anakiita “neno ovu”. “Yeyote amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, akamwoa mwanamke mwingine, azini” (Mathayo 19:9, TLR. Maneno mepesi kutilia mkazo). Machoni pa Mungu, uzinzi ndiyo sababu halali pekee kwa mwanamume kumwacha mke wake. Na ni rahisi kueleweka. Ni kitu gani kingine amb acho mwanamume au mwanamke anaweza kufanya, kikawa kibaya kwa mwenzake kuliko hicho? Mtu anapozini, anatuma ujumbe mchungu sana. Kwa hakika Yesu hakuwa anazungumzia uzinzi tu aliposema hayo. Bila shaka hata kumbusu mwenzi wa mwingine na kumshika-shika ni kitu kibaya sana, kama ilivyo tabia ya kuangalia picha mbaya za ngono, au matendo mengine yasiyofaa ya mahusiano kimwili. Kumbuka kwamba Yesu alifananisha tamaa na uzinzi katika Mahubiri Yake ya Mlimani.
Tusije kusahau Yesu alikuwa anasema na nani – ni Mafarisayo waliokuwa wanaachana na wake zao kwa sababu yoyote na kuoa haraka haraka, lakini hao hao wasingezini kamwe ili wasivunje amri ya saba. Yesu aliwaambia wanajidanganya wenyewe. Walichokuwa wanafanya hakikuwa tofauti na uzinzi. Ndiyo ukweli huo. Yeyote aliye mkweli anaweza kuona kwamba mwanamume anayemwacha mkewe ili amwoe mwanamke mwingine anafanya kitu ambacho mzinzi hufanya. Tofauti ni kwamba, huyu mwingine anahalalisha uzinzi wake.
Ufumbuzi
Huu ndiyo ufunguo wa kulinganisha maneno ya Yesu na ya Musa na ya Paulo. Yesu alikuwa anadhihirisha unafiki wa Mafarisayo tu. Hakuwa anaweka sheria inayozuia kuoa au kuolewa tena. Kama alikuwa anafanya hivyo, basi alipingana na Musa na Paulo, na kusababisha vurugu kwa mamilioni ya watu walioachika, na mamilioni ya watu walioingia kwenye ndoa nyingine. Kama Yesu alikuwa anaweka sheria kuhusu kuoa au kuolewa tena, tuwaambie nini wale ambao wameachika na kuoa au kuolewa tena kabla ya kusikia habari za Sheria ya Yesu? Je, tuwaambie kwamba wanaishi katika mahusiano ya kiasherati? Na, kwa kuwa tunajua Biblia inaonya kwamba hakuna wazinzi au waasherati watakaorithi ufalme wa Mungu (1Wakor. 6:9-10), tuwashauri kwamba waachane na wenzao? Pengine ni sawa, lakini, Mungu si anachukia kuachana?
Je, tuwaambie waachane kitandani mpaka wana ndoa wenzao wa kwanza wafe ili kuwaepusha na zinaa ya kila wakati? Lakini, Paulo si anawakataza wana ndoa kunyimana? Tena, ushauri kama huo si utapelekea watu kujaribiwa kimwili na hata kuamsha hamu za kutaka wana ndoa wenzao wafe?
Je, tuwaambie watu kama hao waachane na wenzao wa sasa na kurudiana na wenzao wa kwanza (kama wengine wanavyosema) – kitu ambacho kinakatazwa na Torati ya Musa katika Kumbukumbu 24:1-4?
Halafu – vipi kuhusu watu walioachana ambao hawajaoa tena? Kama wanaruhusiwa kuoa au kuolewa tena ikiwa wenzao walioachana nao walitenda uzinzi, nani atakayejizatiti kuthibitisha kama kweli uzinzi ulifanyika? Je, itabidi wana ndoa fulani wathibitishe kwamba wenzao walioachana nao walikuwa na hatia ya tamaa tu ili waweze kurudiana? Je, wengine itabidi watafute mashahidi wa kuthibitisha uasherati wa wenzao ili waweze kurudiana?
Kama swali lililopita – vipi kuhusu swala la mwenzi kuzini kwa sababu alikuwa katika ndoa na mtu aliyemnyima tendo la ndoa? Je, ni halali kwa huyo aliyekuwa anamnyima mwenzake tendo la ndoa aruhusiwe kuolewa, na yule mtu aliyezini akatazwe kuoa au kuolewa?
Vipi kuhusu mtu aliyezini kabla ya ndoa? Je, uzinzi wake huo si kukosa uaminifu kwa mwenzi wa baadaye? Je, dhambi hiyo hailingani na uzinzi, kama yeye au mwenzake wangekuwa katika ndoa wakati walipofanya dhambi yao? Mbona huyo aruhusiwe kuoa au kuolewa?
Vipi kuhusu watu wawili wanaokaa pamoja – bila ndoa – halafu wanatengana. Mbona wanaruhusiw akuoa na kuolewa na wengine baada ya kutengana, kwa kuwa hawakuwa na ndoa rasmi? Wana tofauti gani na wale wenye kuachana kisha wakaoa na kuolewa tena?
Vipi kuhusu kweli kwamba “mambo ya zamani yanapita” na “mambo yanakuwa mapya” wakati mtu anapo-okoka (ona 2Wakor. 5:17)? Je, inamaanisha kila dhambi iliyowahi kufanywa isipokuwa dhambi ya kuachana isivyo halali?
Yote hayo na maswali mengine mengi[1] yanaweza kuulizwa, ambayo ni hoja zenye nguvu kabisa kuunga mkono wazo kwamba Yesu hakuwa anaweka sheria mpya kuhusu ndoa. Yesu alikuwa na akili za kutosha kutambua matokeo ya sheria Yake mpya ya ndoa kama ndivyo ilivyokuwa. Hilo tu linatosha kutuambia kwamba alikuwa anaweka wazi unafiki wa Mafarisayo – wanaume wenye tamaa, wanafiki, washika dini, waliokuwa wanaachana na wake zao “kwa sababu yoyote” na kuoa tena.
Sababu ya Yesu kusema kwamba walikuwa “wanazini” badala ya kusema tu kwamba walichokuwa wanafanya ni kosa ni kwa sababu alitaka wao waone kwamba talaka kwa sababu yoyote na kuoa tena baada ya hapo si tofauti na uzinzi, kitu ambacho wao walidai hawafanyi. Je, tuamue kwamba kitu pekee alichojali Yesu ni tendo la ndoa tu katika ndoa ya pili, na kwamba angeunga mkono ndoa ya pili mradi tu watu wasijihusishe katika tendo la ndoa? Hapana. Basi, tusimfanye aseme kitu ambacho hakumaanisha kusema.
Mlinganisho Unaofanya Kufikiri
Hebu tufikiri kuhusu watu wawili. Mmoja ana ndoa, ni mtu wa dini, anayedai kumpenda Mungu kwa moyo wake wote, ambaye ameanza kumtamani mwanamke kijana anayekaa jirani. Muda si muda anamwacha mkewe na haraka anamwoa yule msichana aliyemvutia.
Yule mwingine si mtu wa dini. Yeye hajawahi kusikia hata Injili, na anaishi maisha mabaya ambayo hatimaye yanaharibu ndoa yake. Miaka kadhaa baadaye, akiwa peke yake tu, anaisikia Injili, anatubu, na anaanza kumfuata Yesu kwa moyo wake wote. Miaka mitatubaadaye anampenda mwanamke mwenye kumpenda Mungu sana anayekutana naye kanisani. Wote wawili wanatafuta mapenzi ya Mungu na ushauri wa wengine kwa bidii, kisha wanapanga kuoana. Wanakuja kuonana, na wanakuwa waaminifu kwa Bwana na wao kwa wao mpaka kifo.
Sasa – hebu tudhanie kwamba wote wawili wametenda dhambi kwa kuoa tena. Katika hao wawili, ni yupi mwenye dhambi kubwa zaidi? Bila shaka ni yule wa kwanza. Yeye ni sawa na mzinzi tu.
Lakini – vipi kuhusu yule mtu wa pili? Je, ni kwamba ametenda dhambi? Je, tunaweza kusema kwamba yeye hana tofauti na mzinzi – kama yule wa kwanza? Hapana. Je, tumwambie yale ambayo Yesu alisema kuhusu watu wanaoachana na kuoa tena, na kumjulisha kwamba sasa anaishi na mwanamke ambaye Mungu hakumwunganisha naye kwa sababu anamhesabu bado ana ndoa na mke wake wa kwanza? Je, tumwambie kwamba anaishi katika zinaa?
Majibu yako dhahiri kabisa. Uzinzi hutendwa na watu ambao wameoana, wanaomwona mwingine asiyekuwa mwenzi wao. Kwa hiyo, kuachana na mwenzako kwa sababu umepata mrembo zaidi ni sawa na uzinzi. Lakini, mtu ambaye hajaoa hawezi kufanya uzinzi kwa sababu hana mwenzi wa kumkosea uaminifu, na mtu ambaye ameachika hawezi pia kutenda uzinzi kwa sababu hana mwenzi wa kumkosea uaminifu. Tukielewa mantiki ya kihistoria na kiBiblia kuhusu maneno ya Yesu, hatuwezi kufikia maamuzi yatakayopotosha watu, na yenye kupingana na Maandiko yote.
Wanafunzi waliposikia itikio la Yesu kwa jibu la Mafarisayo, walijibu hivi, “Kama mahusiano ya mwanamume na mke wake yako hivyo, ni afadhali kutokuoa” (Mathayo 19:10, TLR). Tambua kwamba walikuwa wamekulia chini ya mafundisho na ushawishi wa Mafarisayo, na katika utamaduni uliokuwa umeathiriwa sana na Mafarisayo. Hawakuwahi kudhani kwamba ndoa ni kitu cha kudumu kiasi hicho. Ukweli ni kwamba, muda mfupi uliopita, hata wao waliamini ni halali kwa mwanamume kumwacha mkewe kwa sababu yoyote. Basi kwa haraka wakaamua kwamba ingekuwa bora kuepukana na ndoa kabisa, ili kuepuka hatari ya kuachana na kuingia kwenye uzinzi. Yesu alijibu hivi:
Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee (Mathayo 19:11-12).
Yaani – kinachoamua ni ile hamu ya kushirikiana kimwili aliyo nayo mtu, au uwezo wake wa kuitawala. Hata Paulo alisema hivi: “NI afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa” (1Wakor. 7:9, TLR). Wale waliozaliwa wakiwa matowashi au wale wanaofanywa matowashi na watu (kama ilivyokuwa zamani: watu waliwafanya wanaume wengine kuwa matowashi, ili wawape jukumu la kuwalinda wake zao) hawana hamu ya kushirikiana na mwanamke kimwili. Wale “wanaojifanya wenyewe kwa ajili ya ufalme wa mbinguni” ni wale ambao wamejaliwa na Mungu kipekee kuwa na uwezo wa kujitawala zaidi. Ndiyo maana “si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa” (Mathayo 19:11).
Mahubiri Ya Mlimani
Tusisahau kwamba wale watu Yesu aliosema nao wakati akihubiri Mlimani pia walikuwa wameishi maisha yao chini ya ushawishi wa Mafarisayo wanafiki, waliokuwa viongozi na waalimu wa Israeli. Kama tulivyokwisha jifunza hapo mapema tulipotazama Mahubiri ya Mlimani, ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya yale ambayo Yesu alisema yalikuwa kama masahihisho tu ya mafundisho ya uongo ya Mafarisayo. Yesu hata aliwaambia watu kwamba hawataingia mbinguni ikiwa haki yao haitazidi ile ya waandishi na Mafarisayo (Mathayo 5:20), ambayo ilikuwa njia nyingine ya kusema kwamba waandishi na Mafarisayo walikuwa njiani kwenda jehanamu. Mwisho wa mahubiri yake, watu walishangazwa kwa sehemu kwa sababu Yesu alikuwa anafundisha kitofauti, “si kama waandishi wao” (Mathayo 7:29, TLR).
Mapema katika mahubiri Yake, Yesu aliweka wazi unafiki wa wale waliodai kwamba hawajawahi kuzini, ila wanatamani na kuachana na wenzi wao na kuoa tena. Akapanua maana ya uzinzi kwamba ni zaidi ya tendo la kimwili la dhambi baina ya watu wawili walio na ndoa. Na aliyosema yalikuwa wazi kabisa kwa yeyote mwenye akili nzuri na mkweli, ambaye angefikiri kidogo tu. Lakini kumbuka kwamba, mpaka wakati wa mahubiri ya Yesu, wengi wa watu katika lile kundi wangekuwa na mawazo kwamba ilikuwa halali kwao kuachana “kwa sababu yoyote” ile. Yesu alitaka wafuasi Wake pamoja na wengine wote wajue kwamba kusudi la Mungu tangu mwanzo lilikuwa kiwango cha juu zaidi.
Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Usizini’. Lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamey mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanamu. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanmum. Imenenwa pia, ‘Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka.’ Lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya usherati, amfanya kuwa mzinzi, na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini (Mathayo 5:27-32).
Kama tulivyokwisha ona mapema, ona kwamba maneno ya Yesu kuhusu talaka na kuoa tena yanafuata moja kwa moja maagizo aliyotoa kuhusu tamaa, hivyo kuyaunganisha pamoja. Tena, Yesu anasema vyote viwili ni uzinzi, na kuviunganisha zaidi. Basi tunaona kwamba kuna muunganiko wa kitu kinachofanana katika maelezo hayo ya fungu hili lote la Maandiko. Yesu alikuwa anawasaidia wafuasi Wake kuelewa maana ya kutii amri ya saba. Maana yake ni kutotamani, na kutoachana na kuoana tena.
Kila mtu katika wasikilizaji Wake wa Kiyahudi alikuwa amesikia amri ya saba ikisomwa katika sinagogi (maana hawakuwa na Biblia binafsi siku zile), pamoja na mafafanuzi yaliyotolewa, na kuona jinsi waalimu wao – waandishi na Mafarisayo – walivyoyafanyia kazi maishani mwao. Ndipo Yesu akasema, “lakini mimi nawaambia”, ila hakuwa anataka kuongeza sheria zingine mpya. Yeye alitaka kudhihirisha tu mpango wa Mungu tokea mwanzo.
Kwanza – tamaa ilikuwa inakatazwa kabisa na amri ya kumi, na hata bila amri ya kumi, yeyote aliyefikiri vizuri angetambua kwamba ilikuwa ni kosa kutamani kufanya kitu ambacho Mungu amekataza.
Pili – tangu mwanzoni kabisa mwa kitabu cha Mwanzo, Mungu aliweka wzi kwamba ndoa ilitaiwa kuwa makubaliano ya maisha yote. Tena, yeyote aliyefkiri vizuri juu ya hilo angetambua kwamba kuachana na kuoana tena ni sawa tu na uzinzi, hasa kama mmoja atapanga kumwacha menzake kwa kusudi la kuoa tena.
Lakini tena katika mahubiri haya, ni wazi kwamba Yesu alikuwa anawasaidia tu watu waone ukweli kuhusu tamaa na ukweli kuhusu kuachana kwa sababu yoyote, na kuoana tena. Yeye hakuwa anaweka sheria mpya ya kuoana tena ambayo haikuwa “vitabuni” hadi wakati huo.
Inashangaza kwamba ni watu wachache sana kanisani ambao wamewahi kutimiza maneno ya Yesu ya kung’oa jicho au kukata mikono, maana mawazo hayo yanapingana sana na Maandiko mengine, na ni dhahiri kwamba kazi yake ni kutia nguvu hoja kuhusu kuepukana na kujaribiwa kuwa na mahusiano kimwili yasiyofaa. Lakini wengi sana kanisani wanajaribu kutafsiri moja kwa moja maneno ya Yesu juu ya yule mwenye kuoa au kuolewa tena kufanya uzinzi, hata ingawa tafsiri hizo zinapingana moja kwa moja na Maandiko mengine. Lengo la yesu lilikuwa kuwafanya wasikilizaji Wake wakabiliane na ukweli, kwa tumaini kwamba talaka zingepungua baada ya hapo. Kama wafuasi Wake wangepkea moyoni yale aliyosema kuhusu tamaa, kusingekuwepo na uasherati au uchafu miongoni mwao. Kama usingekuwepo, kusingekuwepo na sababu halali za talaka. Basi, talaka isingekuwepo, kama Mungu alivyokusudia tangu mwanzo.
Mwanamume Anamfanyaje Mkewe Azini?
Ona maneno ya Yesu, kwamba, “Yeyote amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi.” Hili tena linatufanya tuamini kwamba hakuwa anaweka sheria mpya ya kuoana tena, bali alikuwa anadhihirisha tu ukweli kuhusu dhambi ya mtu anayemwacha mkewe bila sababu nzuri. “Amfanya kuwa mzinzi.” Kuna wanaosema kwamba Yesu alikuwa anamzuia huyo mwanamke kuolewa tena, kwa sababu anasema huo ni uzinzi. Lakini si hivyo. Mkazo uko kwenye dhambi ya mwanamume anayemwacha mkewe, kwamba, kwa sababu ya kile anachokitenda, mke wake atakuwa hana lingine la kufanya isipokuwa kuolewa tena, ambayo si dhambi kwa upande wake maana yeye ameathirika kutokana na ubinafsi wa mumewe. Machoni pa Mungu ni kwamba, kwa kuwa mwanamume alimwacha mkewe na kumwingiza kwenye kuolewa tena, ni kama amemlazimisha aingie kitandani na mwanamume mwingine. Basi, yule anayedhani hajatenda uzinzi anakuwa na hatia kwa uzinzi mara mbili – wa kwake na wa mkewe.
Yesu hakusema kwamba Mungu anamhesabu mke aliyeathiriwa na talaka kwamba ana hatia ya uzinzi, maana hiyo isingekuwa halali, tena ingekuwa haina maana kabsia kama huyo mke aliyeathiriwa asingeolewa. Mungu angewezaje kusema kwamba ni mzinzi kama asingeolewa? Isingekuwa na maana kabisa. Basi, ni dhahiri kwamba Mungu anamhesabu huyo mwanamume kuwa na hatia kwa uzinzi wake mwenyewe na “uzinzi” wa mkewe, ambao kweli si uzinzi kwake maana ni ndoa ya pili ambayo ni halali kabisa.
Sasa – vipi kuhusu maneno ya Yesu yafuatayo kwamba, “na mtu akimwoa mwanamke aliyeachwa anazini”? Ni mawili tu yanayoweza kueleweka. Aidha Yesu alikuwa anaongeza hatia ya uzinzi wa tatu dhidi ya mtu anayedhani kwamba hajawahi kuzini (kwa sababu ile ile kama aliyotumia kuongeza hatia ya pili), au Yesu alikuwa anasema kuhusu huyo mwanamume anayemtia moyo mwanamke aachane na mumewe ili waoane, “asizini”. Kama Yesu alikuwa anasema kwamba mwanamume yeyote duniani anayemwoa mwanamke aliyeachwa anazini, basi kila mwanamume wa Israeli alizini katika kipindi cha miaka mia nyingi ambaye, katika kutimiza Torati ya Musa, alimwoa mwanamke aliyeachika. Ukweli ni kwamba kila mwanamume siku hiyo aliyekuwa anamsikiliza Yesu, aliyekuwa amemwoa mwanamke aliyeachika kwa kufuatana na Torati ya Musa, alikuwa na hatia ya kosa ambalo hakuwa na hatia yake muda mfupi kabla ya hapo, na Yesu akawa amebadilisha sheria ya Mungu hapo hapo. Tena, kila mtu katika wakati ujao ambaye alimwoa mtu aliyeachwa, kwa kuamini neno la Paulo katika barua yake kwa Wakorintho kwamba hilo si dhambi, alikuwa ametenda dhambi – ni mzinzi.
Jinsi Biblia ilivyo inapelekea mtu kumstahi sana mwanamume aliyeoa mwanamke aliyeachwa. Kama yeye ni mwathirika wa ubinafsi wa mume wake wa kwanza, asiye na hatia, ningemstahi sana mwanamume huyo, kama ambavyo ningemstahi sana mwanamume anayeoa mjane na kumtunza. Kama huyo mwanamke alikuwa na sababu ya kulaumiwa kwa talaka yake, bado ningemstahi sana kwa kuwa na moyo wa Kristo kwa kuamini kwamba kuna kilicho bora kwake, na kwa neema yake ya kukubali kusahau yaliyopita na kujaribu. Kwa nini mtu yeyote aliyesoma Biblia, mwenye Roho Mtakatifu ndani yake aamue kwamba Yesu alikuwa anamkataza kila mtu asioe au kuolewa na yeyote aliyeachika? Hilo linaingiaje kwenye ukweli kwamba Mungu ni mwenye haki – haki ambayo haimwadhibu yeyote kwa kuwa mwathirika – kama mwanamke ambaye anaachwa pasipo kuwa na kosa? Hoja kama hiyo inaingiaje kwenye ujumbe wa Injili, wenye kutoa msamaha na nafasi nyingine kwa wenye dhambi wanaotubu?
Kuhitimisha
Biblia inasema tena na tena kwamba talaka inahusisha dhambi kwa mmoja au kwa wenzi wote wawili. Mungu hakukusudia mtu yeyote aachane na mwenzake katika ndoa, lakini kwa rehema Zake alitoa mwanya wa talaka kama uasherati ukitokea. Kwa rehema pia aliweka mpango kwa watu walioachika kuoa na kuolewa tena.
Kama si kwa sababu ya maneno ya Yesu kuhusu kuoa na kuolewa tena, hakuna msomaji yeyote wa Biblia ambaye angedhani kwamba kuoa na kuolewa tena ni dhambi (isipokuwa kwa habari za matukio mawili nadra sana katika agano la kale, na moja la nadra sana katika agano jipya, yaani, kuoa na kuolewa tena baada ya mtu kuachana na mwingine aliyeokoka). Ila, tumepata njia inayokubalika ya kulinganisha kile alichosema Yesu kuhusu kuoa na kuolewa tena, na sheria kali zaidi yenye kukataza kuoa au kuolewa tena kwa kila hali. Hii sheria haifanyi kazi kwa wale ambao wamekwisha achana na kuingia katika ndoa zingine (maana ni sawa na kurudisha mayai yaliyopikwa yawe mabichi), na ni moja ambaye ingesababisha mkanganyiko wa hali ya juu na kuwapelekea watu kuvunja sheria zingine za Mungu. Badal ayake, tumeona kwamba Yesu alikuwa anawasaidia watu kutambua unafiki wao. ALikuwa anawasaidia wale walioamini kwamba hawatazini kamwe waone kwamba wlaikuwa wanazini kwa njia zingine, kwa tamaa zao na kwa mtazamo wao mwepesi kuhusu sababu za kuachana.
Kama Biblia nzima inavyofundisha, msamaha hutolewa kwa wenye dhambi wanaotubu, bila ya kujali dhambi yao, na nafasi ya pili na ya tatu hutolewa kwa wenye dhambi – pamoja na walioachika. Hakuna dhambi katika kuoa na kuolewa tena kwa aina yoyote katika agano jipya, isipokuwa kwa mwamini aliyeachana na mwamini mwenzake. Na hilo halipaswi kutokea kwa sababu waamini wa kweli hawafanyi uchafu, na kwa sababu hiyo hakuna sababu halali ya kuachana. Ikitokea kwa nadra, wote wawili wabaki kama walivyo au wapatane.